Marekani imekanusha madai ya Korea Kaskazini kuwa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ametangaza vita dhidi ya taifa lao.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Huckabee Sanders imeeleza kuwa madai hayo sio ya kweli na kuwataka viongozi wa Korea Kaskazini kuacha uchokozi kutokana na kauli yao kuwa itaitungua ndege yoyote ya Marekani popote ilipo kwani imetangaziwa vita.

Kauli hiyo ya Marekani inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Ri Yong-ho kudai kuwa dunia inapaswa kufahamu kwamba itachukua hatua hiyo kwakuwa Marekani ndiyo iliyoanza kutangaza vita.

Yong-ho aliikariri tweet ya Rais Trump iliyosema, “Korea Kaskazini inaweza kupotea muda sio mrefu kama viongozi wake wataendelea na uchokozi wa kufanya majaribio ya mabomu ya nyuklia.”

Akihutubia hivi karibuni kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Rais Trump alisema Marekani itaisambaratisha Korea Kaskazini kama itaendelea na majaribio ya makombora ya nyuklia.

Saa chache baadae, ndege za kijeshi za Marekani zilipita karibu na anga la Korea Kaskazini.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un alijibu hotuba hiyo kwa vitisho zaidi na Serikali yake ikaahidi kujibu mapigo kwa kufyatua kombora zito zaidi la bomu la nyuklia hivi karibuni.

Makao Makuu Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imeonya kuwa endapo Korea Kaskazini itaendelea na mpango wake, itamshauri Rais Trump hatua zaidi za kuchukua.

Nick Minaj akubali mziki wa Cardi B, ampongeza kwa kuvunja rekodi
Video: Tamko la Kenyatta kuhusu maandamano ya NASA