Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire, ameionya Young Africans kuelekea mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Young Africans itacheza dhidi ya Simba SC kwenye mchezo huo Julai 25, Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Masau Bwire ametoa onyo hilo kwa ujumbe maalum na kuusambaza katika mitandao ya kijamii, akianza kwa kuipongeza Young Africans kwa ushindi dhidi ya Simba SC walioupata Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (Julai 03).

Masau ameandika: Kama alivyosema Nabi, Kocha mkuu wa Young Africans, ndivyo ilivyo, Simba ni bora, nami niungane naye kusema ndivyo!

Mbinu aliyoitumia Nabi, kama anavyosema yeye, kuwasoma na kuwaelewa Simba, kuwazuia na kutumia mapungufu, makosa yao kuwafunga ni sahihi kabisa, kwa mwalimu mzuri wa soka, hiyo ndiyo akili na ushindi!

Hongera Nabi, Hongera Young Africans kwa ushindi!

Ila, Wananchi msibweteshwe, mkabweteka kwa ushindi huo, kaeni chonjo, jiandaeni, jipangeni kwa mchezo mwingine wa karibuni, mkirogwa, mkarogeka kwa kujisau, Kigoma kwa Waha, mtaimbwa Yesu asifiwe Msikitini!

Simba SC, poleni kwa matokeo WATANI wa wenyewe, mpira huu wa miguu, ndivyo ulivyo, kubalianeni tu na yaliyotokea, yametokea, yamekuwa, ndivyo imekuwa, hakuna namna nyingine, ni kukubali na kuizoea hali, kazi iendelee!

Ushauri wangu kwenu, kipindi hiki si cha kurushiana mishale, kulaumiana, kushutumiana, na kushambuliana ninyi kwa ninyi, ni kipindi cha kukaa pamoja, kutafakari, kutathimini, kusahihisha, kurekabisha na kutengeneza, ili, katika mchezo ujao siku za karibuni, yasijirudie yaliyotokea!

Usajili wapamba moto Ulaya
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 5, 2021