Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire ameitakia kila la kheri Simba SC kwenye mchezo wake wa Ligj ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC itacheza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana leo Jumapili (Oktoba 17), mjini Gaborone, mchezo utakaoanza majira ya saa tisa kwa saa za Afrika Kusini sawa na saa kumi kwa saa za Afrika Mashariki.

Masau ameitakia kheri Simba SC kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa kuandika waraka ulioambatana na dua ya kuitakia timu hiyo ya Msimbazi ushindi ugenini.

Masau ameandika:

Kila la kheri Simba SC….

Ni saa kadhaa zimesalia, Simba SC iingie uwanjani leo October 17, 2021, huko Botswana kunyukana na Jwaneng Galaxy katika kinyang’anyiro cha mashindano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Wana Simba SC na Watanzania wazalendo, tuungane kwa pamoja kuitakia heri na kuiombea timu yetu hii ya Tanzania ushindi katika mchezo huo.

Simba SC ni timu iliyojikusanyia heshima kwa mafanikio ya soka Afrika kufikia kuwa miongoni mwa timu 10 bora za soka Afrika,  imeitangaza vema nchi yetu na kuiheshimisha katika ubora wa soka Afrika na Dunia.

Watanzania tuna kila sababu  ya kuiombea ushindi na mafanikio zaidi Simba SC,  kwani, kufanikiwa kwake kunasababisha na timu nyingine kufanikiwa, ushiriki wa timu nne katika mashindano ya kimataifa, ni mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na kufanikiwa ya Simba SC.

Yeyote anayeitakia na kuiombea mabaya timu hii,  nitamuona wa ajabu sana, lengo lake siyo zuri kwa maendeleo ya soka la nchi yetu, anataka turudi kule kwa zamani kwenye ushiriki wa timu mbili kimataifa, huyo ni wa kusutwa bila aibu tena hadharani, kweupe kabisa!

Ebu tuipe heshima yake timu hii, tuthamini mchango wake katika mafanikio na maendeleo ya soka la Tanzania, tuache tofauti zetu  za hao ni wa Msimbazi, sisi ni wa huku kwetu, tuiombee ushindi na kusonga mbele zaidi katika mashindano hayo ya ligi ya mabingwa, kwani,  kufanikiwa kwa Simba SC,  kunaleta mafanikio kwa timu yako na nchi yetu kwa ujumla.

*Kila la kheri miamba, ushindi leo ni muhimu*

Mungu ibariki Tanzania,  Mungu ibariki Simba SC.

Mbali na kuiombea Simba SC,  ipate ushindi leo, tuendelee kuwaombea Azam FC na Biashara United wafanye vizuri, wavuke hatua hii, waingie hatua nyingine ya mashindano ya shirikisho Afrika wanayoshiriki.

Simba SC nguvu moja.
Masau Kuliga Bwire – Mzalendo.

Mwanza kunufaika na Uongozi wa Rais Samia
Young Africans yaenda Songea