Baada ya kuambulia alama moja kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara juzi Jumanne (Desemba 28), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire ameoneshwa kukerwa na Mwamuzi wa pambano hilo, lililounguruma kwenye Uwanja wa Azam Complex Jijini Dar es salaam.

Ruvu Shooting walitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Ally Kombo dakika ya 22, kabla ya Charles Ilamfya hajaisawazishia KMC FC dakika za lala salama.

Masau Bwire amesema anaamini Ruvu Shooting ilikua na kila sababuza kuondoka na alama tatu za mchezo huo, lakini Mwamuzi aliongeza muda zaidi na kuwawezesha KMC kupata sare hiyo jambo ambalo anaamini hawakutendewa haki.

Amesema waamuzi wanaua soka la Tanzania kutokana na maamuzi yao ya hovyo wanayoyatoa kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Siku zote tunalia na maamuzi ya waamuzi, mwamuzi aliwaongezea muda zaidi KMC na wakasawazisha bao,” amesema Bwire.

“Mwamuzi alionyesha wazi kabisa kuibeba KMC, kwani baada ya kuongeza muda zaidi na lilipofungwa tu bao na yeye akamaliza mchezo, hii si sawa kabisa, waamuzi wanaua soka la Tanzania.”

“Kwa maamuzi haya, kuna siku anaweza kutokea mtu akiwa na hasira na akafanya jambo la hatari sana. Kwa nini kila siku tunalia na waamuzi lakini hakuna hatua zinazochukuliwa?” amehoji Masau Bwire

Kwa matokeo hayo, KMC imefikisha alama 11 ikiwa katika nafasi ya 12 na Ruvu Shooting sasa ina alama 10 katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Klopp: Tulistahili kufungwa
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 30, 2021