Israel imeendelea kufanya mashambulio kwenye Ukanda wa Gaza mfululizo huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kuitisha kikao cha dharura ikiwa ni juhudi kubwa za kidiplomasia zenye lengo la kusimamisha mashambulizi yanayofanywa na ndege za Israel ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 200.
Kiongozi wa Maseneta wa Chama cha Republican nchini Marekani, Seneta Mitch McConnel amemtaka Rais Joe Biden asimame imara katika kuiunga mkono Israel, hata hivyo Rais Biden amesema anaunga mkono pendekezo la kusimamisha mapigano lakini hakutamka wazi kuitaka Israel iache kufanya mashambulizi.
Kwa upande mwingine wapiganaji wa Kipalestina wameendelea kuishambulia Israel kwa makombora ya mara kwa mara hadi ndani ya Nchi hiyo ikiwa leo ni siku ya 8 tangu kuibuka kwa mashambulizi ya hivi karibuni.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya kikao cha dharura katika muktadha wa juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kusimamisha mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas kwenye Ukanda wa Gaza.
Kikao hicho cha Baraza la Usalama ambacho ni cha nne tangu mgogoro uanze, kimeitishwa baada ya Marekani ambaye ni mshirika mkuu wa Israel kuzuia kwa mara ya tatu kupitishwa tamko la pamoja juu ya kutaka mapigano yasimamishwe.
Hata hivyo rais Joe Biden amemwambia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba Marekani inaunga mkono pendekezo la kusimamisha mapigano lakini hakutamka wazi kuzitaka pande zote ziweke silaha chini.
Wakati huo huo ofisi ya rais nchini Ufaransa imefahamisha kwamba rais Emmanuel Macron atafanya mazungumzo na rais wa Misri pamoja na mfalme wa Jordan ili kutafuta njia ya kusitisha mapigano baina ya Israel na wapiganaji wa Hamas.
Kutokana na mashambulio ya ndege za Israel wapalestina 213 wameshauawa, miongoni mwao watoto 61 huku Wapalestina wengine 1400 wamejeruhiwa.
Kwa upande wao wapiganaji wa Hamas wamerusha makombora 3500 yaliyosababsiha vifo vya Waisrael 10 miongoni mwao mtoto mmoja.
Israel imefungua mpaka wa Karem Shalom kuruhusu mahitaji ya kibinadamu kuingia Ukanda wa Gaza.