Kocha Mkuu wa Klabu ya Dodoma Jiji FC Masoud Djuma Irambona amewataka radhi Mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kikosi chake kuanza vibaya Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Dodoma Jiji FC ilianza msimu kwa kupokea vipigo kutoka kwa Tanzania Prisons na Mbeya City FC, zote kutoka mkoani Mbeya.
Kocha Masoud amesema hana budi kuwataka radhi Mashabiki wa Dodoma jiji FC kwa matokeo hayo ambayo hakuyatarajia, lakini akaahidi kupambana vilivyo na kuirudisha timu yake katika furaha ya ushindi.
“Nikiri kwamba tumekua na mwanzo ambao hatukuutarajia, kupoteza michezo miwili ya kwanza tukiwa nyumbani ni jambo baya, lakini tunajipanga kuona tunabadili matokeo, na kupata matokeo ya furaha.”
Kocha huyo kutoka nchini Burundi ameeleza kuwa kilichochangia washindwe kufanya vizuri katika michezo hiyo miwili ni muda mfupi walioupata, wakati wa maandalizi ya msimu.
Amesema asilimia kubwa ya wachezaji wanaoanza kwenye kikosi chake cha kwanza ni maingizo mapya, hivyo ilihitaji muda wa kutosha kuweza kujenga muunganiko mzuri na kupata matokeo ya ushindi.
Amesema pamoja na yote, ligi bado ni mbichi, ana uhakika wa kurekebisha makosa yao na kufanya vizuri katika michezo ijayo ya Ligi na Michuano ya Kombe na Shirikisho ‘ASFC’.