Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar wameanza kikao cha siku tatu kwa ajili ya kufanya tathmini kwa kazi zilizofanyika kwa mwaka 2022 na kuweka mikakati Madhubuti kwa mwaka 2023.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa amewataka Watendaji hao kuendelea kufanya kazi kwa kasi ili kuhakikisha kuwa kila anayefanya vitendo vya Ukatili anakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Amesema, Jeshi la Polisi linatakiwa kuendelea kujenga majengo ya madawati katika maeneo ambayo hayapo, ili wahanga wa vitendo vya ukatili waweze kuripoti matukio hayo bila ya kupata changamoto ikiwemo ya kuona aibu.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Maria Nzuki alisema kikao hicho kimekuwa kikifanyika kila mwaka na kimeendelea kuwa na mafanikio kutokana na kuwa na mikakati na maazimio ambayo yamekuwa yakitekelezwa ili kupunguza vitendo vya ukatili nchini.
Amesema, mpaka sasa kuna madawati 420 nchini ambapo watendaji wote katika madawati hayo wamepatiwa mafunzo maalumu ambayo yamewasaidia kutoa huduma bora kwakushirikiana na wadau wengine katika mapambano dhidi ya ukatili.
Awali, Mwakilishi wa Shirika la LSF Bi. Jane Matinde amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha kuwa linawafikia watu wengi Zaidi hususani katika kuharakisha upelelezi na kutoa mafunzo kwa watendaji wa Dawati ili waweze kutoa huduma bora kwa wahanga wa ukatili.