Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefanyika jijini Bujumbura, Burundi hivi karibuni.

Waziri wa Ulinzi wa Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Alain Tribert Mutabaze, amesema jitihada za pamoja ikiwemo mikakati mipya ya namna ya kukabiliana na vikundi vya waasi katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado zinahitajika ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.

Amesema “pamoja na kupongeza jitihada nyingi zinazofanywa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kupeleka Kikosi cha Kulinda amani cha Jumuiya (EACRF), bado ipo haja ya
kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mikakati iliyopo kama inaleta tija na kuandaa mikakati mipya ikiwa ni pamoja na kuviwezesha Vikosi hivyo ili viweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kulinda amani katika eneo hilo.”

Aidha, Mutabaze ameongeza kuwa “changamoto katika eneo la Mashariki mwa Congo bado zipo. Tunatakiwa kuboresha mikakati yetu na kufanya tathmini za mara kwa mara ya maendeleo ya jitihada hizi, kwani hali inayoendelea Mashariki mwa Congo inatuathiri sote kama jumuiya kwa namna moja au nyingine. Hivyo niwaombe Waheshimiwa Mawaziri tuje na mapendekezo yenye tija tutakayoyawasilisha kwa Wakuu wetu wa Nchi kwa mustakabali wa eneo hilo la Mashariki mwa Congo na sisi sote.”

Wawili Young Africans watangulia Algeria
Maguere ruhsa kuondoka Manchester United