Mashambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele anaamini atakuwa na nafasi nyingine ya kuisaidia timu yake kupata matokeo chanya katika Uwanja wa nyumbani dhidi ya As Real Bamako ya Mali.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa baadae leo Jumatano (Machi 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa moja usiku.
Mshambuaji huyo ambaye aliifungia bao Young Africans ikicheza ugenini dhidi ya AS Real Bamako mwishoni mwa mwezi Februari amesema, Uwanja wa Machi 26 uliotumika kwa mchezo huo haukuwa rafiki, hivyo ilikua ngumu kufikia lengo la kuchomoza na ushindi mkubwa, na badala yake wakaambulia sare ya 1-1.
“Kiufundi uwanjani tuliotumia katika mchezo wa kwanza ugenini huko Mali ulitufanya tushindwe kucheza aina ya soka letu tulilolizoea la mipira mirefu kwenda goli la wapinzani wetu.”
“Kwani uwanja huo ulikuwa mdogo, hivyo basi wamekuja kwenye uwanja wetu wa Mkapa, basi niwaondoe hofu kuwa hatutawaacha hapa ni lazima tuwafunge.”
“Niwaahidi mashabiki kuwa, tutaingia uwanjani kwa ajili ya kupata ushindi pekee na sio kitu kingine ili tujiweke katika nafasi nzuri nzuri katika msimamo wa kundi letu,” amesema Mayele.
Young Africans itahitaji kushinda mchezo wa leo dhidi ya AS Real Bamako ili kujiweka kwenye mazigira mazuri ya kufuzu Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Hadi sasa Young Africans imekusanya alama 04 baada ya kucheza michezo mitatu ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C, ikitanguliwa na AS Monastir ya Tunisia yenye alama 07.
TP Mazembe ya DR Congo ipo nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 03, na AS Real Bamako inaburuza mkia wa Kundi C ikikusanya alama 02.