Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Mbeya City Shah Mjanja, ameonyesha kushangazwa na maamuzi ya Mwamuzi Ester Adalbert kwa kumuonesha kadi nyekundu Samson Madeleke, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC.
Mbeya City ilicheza ugenini Uwanja wa Benjamin Mkapa jana Jumatano (Januari 18), ikiambulia kichapo cha mabao 3-2.
Shah amesema Mwamuzi Ester hakupaswa kutoa adhabu ya Kadi ya pili ya njano iliyozaa Kadi nyekundu kwa Mdeleke, kwa sababu tayari kikosi chao kilikua kikiongozwa kwa mabao matatu.
Amesema tukio lililofanywa kwa Beki huyo dhidi ya Pape Ousman Sakho halikuwa kubwa kihivyo, kwa hiyo mwamuzi alipaswa kutumia busara ili kuinusuru Mbeya City.
“Sifahamu hekima ambayo Muamuzi wa kati ameitumia na kumpatia kadi ya njano ya pili na kumtoa Beki wetu Samson Madeleke, kwa sababu, tayari Simba alikua anaongoza goli 3 dhidi yetu”
“Pili, dhoruba husika ilikua ni ndogo sana kiasi kwamba katika kuacha mchezo uwe wa ushindani hakukua na sababu yenye uzito wa kumtoa kwa kadi nyekundu”
“Ukimuondoa mchezaji mmoja tena beki katika mchezo muhimu kama huu, unatuondolea na kutupunguzia uwezo wetu wa kushindana uwanjani.” amesema Shah
Katika hatua nyingine Shah Mjanja amelalamika akidai Penati ambayo Simba SC iliipata na kuzaa bao la pili haikuwa halali.
Kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Mbeya City, Simba SC imefikisha alama 47 zinazoendelea kuwaweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakitanguliwa na Young Africans yenye alama 53. Mbeya City inaendelea kusalia nafasi ya 10, ikiwa na alama 21.