Hatimaye mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoa neno kuhusu kupotea kiutata kwa msaidizi wake, Bernard Saanane.

Akizungumza jana katika uchaguzi wa viongozi wa kanda ya Nyasa (Mbeya, Iringa, Songwe, Rukwa na Njombe), Mbowe amesema kuwa amekuwa kimya tangu zitolewe taarifa za kupotea kwa Saanane kwakuwa suala hilo liko katika hatua za uchunguzi.

“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea wale ambao wamemteka wanaweza hata kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema.

Aliongeza kuwa Chadema kama Taasisi yenye idara za ulinzi na usalama kwa upande wake pia inaendelea kufanya uchunguzi kubaini nini hasa kilichojiri katika tukio hilo.

Mbowe alieleza kuwa yeye pia kama viongozi wengine wa chama hicho wameumizwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wa Saanane pamoja na ndugu zake.

Katika uchaguzi huo, Mchungaji Peter Msigwa alishinda nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 62 kati ya 106, sawa na asilimia 58.49. Sadrick Malila alitangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti aliyeshinda kwa asilimia 88 ya kura zote.

 

PolePole: Tunafanya mageuzi ya makusudi ndani ya CCM
Sakata la ‘Kuskani’ Makontena Bandarini laibuka na mapya