Serikali nchini, imetakiwa kuwa makini na kanuni zitakazotungwa kwenye muswada wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi wa mwaka 2022, na kuhakikisha zinaenda sambamba na matakwa ya sheria ili kuondoa sintofahamu na malalamiko kwa jamii.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu wakati akichangia mada Bungeni jijini Dodoma hii leo Novemba 2, 2022.
Amesema, sheria hiyo ni nzuri lakini utungaji wa kanuni zake unatakiwa kuendana na sheria iliyopitishwa kitu ambacho kitasaidia kuondoa mkanganyiko kwani bila uangalifu linaweza kusababisha ugumu wa utekelezaji wake.
“Pamoja na sheria hii kuwa nzuri na tumekuwa tukipitisha hapa, kumekuwa na changamoto ya kanuni, niombe sana kwenye eneo hili na sisi tunamuamini Waziri, sheria ikitungwa nzuri iende hivyo hivyo na kanuni ziwe nzuri,” amefafanua Mtaturu.
Mtaturu ameongeza kuwa, “Tumekuwa tukipitisha baadhi ya sheria lakini ile nafasi ya kutengeneza kanuni huwa inakwenda kuharibu kabisa sheria, matokeo yake wabunge tunaulizwa mlipitishaji sheria hii, kumbe kanuni imekwenda kuharibu maudhui ya sheria ambayo tumeipitisha.”
Hata hivyo, Mtaturu amemuomba Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson kuruhusu kanuni hizo zijadiliwe Bungeni ili wajiridhishe kabla hazijaanza kutumika huku akisema muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022, utaongeza idadi ya wawekezaji na wigo wa ajira nchini.