Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Viti Maalum (Chadema) akiwakilisha walemavu, Dkt. Elly Macha amefariki dunia leo hii nchini Uingereza alipokwenda kwa ajili ya matibabu.
Dkt. Macha amefariki katika hospitali ya New Cross, Wolverhampton nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kuja nchini ikiwa ni pamoja na taratibu za mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
Aidha, kufuatia msiba huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai ameahirisha vikao vya kamati vilivyokuwa vinaendelea hadi kesho Jumamosi, Aprili Mosi, 2017.
Pia, Tumaini Makene ambaye ni msemaji wa Chadema amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, ambapo amesema mbunge huyo awali alikuwa akipatiwa matibabu mkoani Arusha.
  “Taarifa ni za kweli, mbunge Viti Maalum Dkt. Elly Macha amefariki, lakini sijapata bado taarifa za kina, lakini ninachojua ni kwamba amekuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu Arusha” Amesema Makene
Naye Mbunge, Lazaro Nyalandu kupitia mtandao wa twitter ameandika – “Mbunge mwenzetu, Mhe. Dr. Elly Macha amefariki dunia leo. Wabunge wote tumeguswa sana na tukio hilo. Upumzike kwa amani dada yetu mpendwa”

Ibrahimovic Awashusha Presha United
Filamu ya ‘The Dark Tower’ ya Idris Elba yatupwa mbele