Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amezindua boti ya utalii iitwayo TAWA SEA CRUISER, katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, yaliyopo katika Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mchengerwa amewataka wananchi kutumia boti hiyo itakayounganisha shughuli za utalii katika kanda ya kusini na ukanda wa pwani, ili kuendelea kukuza utalii wa ndani.
Boti hiyo, TAWA SEA CRUISER yenye uwezo wa kubeba watalii 50 kwa mara moja, imelenga kuimarisha shughuli za usafirishaji wa watalii wanaotembelea katika Hifadhi ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Aidha, Waziri Mchengerwa pia amepokea Meli ya Kimataifa ya watalii iitwayo, LE JACQUES – CARTIER PONANT iliyobeba watalii 90 kutoka nchi ya Ufaransa na Marekani ikiwa ni meli ya tatu ya Kimataifa iliyotia nanga katika Hifadhi za Magofu ya Kilwa Kisiwani, ndani ya kipindi cha wiki moja.