Mkuu wa Benchi la ufundi la Kagera Sugar Mecky Mexime, ameendelea kuwachimba mkwara Young Africans, ambao atakutana nao leo usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam katika mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mexime alianza kuwachimba Mkwara Young Africans tangu jana, baada ya kukamilisha maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa leo, ambao umepangwa kuanza mishale ya saa moja usiku.

Kocha huyo ambaye aliwahi kutamba na Mtibwa Sugar wakati akisakata kabumbu, amesema kuna haja ya mashabiki kujitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mpambano huo na kuona burudani na namna watakavyozichukua alama tatu muhimu kutoka kwa Young Africans.

Maxime amesema kutokana na maandalizi aliyoyafanya kwa wachezaji wake, anaamini mambo yatamnyookea mbele ya Young Africans, ambao amedai ameshawasoma na kutambua udhaifu wao.

“Walikuja nyumbani wakatufunga na kuchukua pointi tatu, basi nasi tumekuja kwa Mkapa tunahitaji pointi tatu na tutatoa burudani.

“Unajua kwetu sisi ni mara chache kuingia ndani ya Uwanja wa Mkapa, sasa tumekuja nasi tunahitaji kuwafuata pale juu ambapo wapo.

“Mbinu ya kuwafikia ni moja tu kupata ushindi ndani ya uwanja na kupata pointi tatu, mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti na kuona burudani,” amesema.

Kagera Sugar inakutana na Young Africans iliyo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imecheza michezo 19 na kukusanya alama 45.

Kagera Sugar yenyewe imejijengea ngome nafasi ya 10 ikiwa na alama 23 baada ya kucheza michezo 19.

Imetoka kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Gwambina, Uwanja wa Kaitaba kwa bao la mshambuliaji wao namba moja Mhilu Yusuph mwenye mabao matano.

Leo inakutana na kinara wa Young Africans kwa utupiaji wa mabao Deus Kaseke ambaye alitupia kwenye mchezo wa mwisho walipocheza Mbeya mbele ya Mbeya City kwenye sare ya kufungana bao 1-1.

Walipokutana Uwanja wa Kaitaba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Kagera Sugar ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na kuziacha pointi tatu mazima.

TZ Prisons, Mbeya City waiponza Young African, yapigwa faini TPLB
Namungo FC: Figisu za Angola zimetupa somo zito