Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema) ameeleza sababu zilizopelekea viongozi wa Manispaa za jiji la Dar es Salaam zinazoshikiliwa na chama hicho kutohudhuria katika ziara ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.

Makonda alifanya ziara yake hivi karibuni mkoani humo ambapo alisikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa kadri alivyoona inafaa.

Akizungumza leo na Magic FM, Meya huyo amesema kuwa hawakuweza kuonekana katika ziara hiyo kama viongozi kwa kuwa hawakupata mualiko wowote na hawakushirikishwa kufahamu kitakachofanyika katika ziara hiyo.

“Itoshe tu kusema kwamba kama tungehitajika kuonesha ushirikiano tungefanya hivyo,” alisema.

“Lakini unapoanza ziara mwenyeji si unamtaarifu?” alihoji. “Sasa mimi sikutaarifiwa kwamba kuna shughuli gani au kuna jambo gani, labda lilikuwa jambo lake la kazi binafsi ndio maana hatukuweza kualikana kwamba anataka kufanya jambo hilo,” aliongeza.

Meya huyo alisema kuwa kilichofanywa kwao ni kama kushtukizwa tu jambo ambalo amedai sio jema baina ya viongozi.

Martin Saanya Na Wenzake Wawekwa Pembeni
Safari Ya Kuijenga Serengeti Boys Mpya Kuanza Kesho