Mfalme Goodwill Zwelithini wa Zulu amesema kuwa kitendo cha baadhi ya serikali za Afrika kuzuia adhabu ya viboko mashuleni kumesababisha kushuka kwa nidhamu na kuporomoka kwa kiwango cha elimu.
Kwa mujibu wa CNN, Mfalme Zwelithini ameyasema hayo jana alipokutana na viongozi wa ngazi za juu katika sekta ya elimu wa KwaZulu-Natal ambako ni eneo analolitawala.
Mfalme huyo alisisitiza kuwa adhabu ya viboko husaidia watoto kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao kwa kuwa inawasukuma kujifunza kwa bidii.
“Haya mambo [ya kuzuia adhabu ya viboko mashuleni] yanatuangusha kwa sababu watoto hawawi na nidhamu,” alisema.
Afrika Kusini ilipiga marufuku adhabu ya viboko mashuleni tangu mwaka 1997, ingawa inaendelea katika baadhi ya shule kinyume cha sheria.
Kauli ya Mfalme huyo imekuja baada kipande cha video kinachomuonesha mwalimu mmoja akimchapa viboko mwanafunzi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Serikali ya nchi hiyo ililaani vikali kitendo hicho na kuahidi kumchukulia mwalimu huyo hatua kali.
Katika hatua nyingine, Mfalme huyo alilaani mauaji ya mwalimu mmoja yaliyotokea katika eneo la Gauteng ambalo ni eneo muhimu zaidi kwa uchumi wa Afrika Kusini.
Aliwataka walimu kuundiwa tume maalum ya kusikiliza malalamiko yao na kulinda usalama wao. Pia, aliitaka Serikali kuchukua hatua sawa na zile zinazochukuliwa mwanasiasa anapouawa.