Hospitali zote na vituo vya afya nchini zimeagizwa kutoa damu kwa Mgonjwa mwenye uhitaji huku wataalamu wa afya wakisisitizwa kuendelea kutoa elimu kuhusu uchangiaji damu kwa hiari, kupitia vituo vya Kanda, Mikoa, Halmashauri na maeneo yatakayokuwa yameandaliwa kwa ajili ya uchangiaji damu.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri Dkt. Dorothy Gwajima wakati akimuwakilisha katika maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri huyo ameagiza Timu za kukusanya damu za kila ngazi Kanda, Mikoa, Halmashauri na Vituo maalumu kujikita kwenye kukusanya damu kutoka kwa wachangia damu wa hiari na kuhakikisha uwepo wa damu ya kutosheleza mahitaji muda wote huku akikisitiza kuwepo ajenda ya kudumu ya uwepo wa damu salama kwenye vikao vya uongozi katika ngazi zote.
“Naomba Usimamizi dhabiti wa matumizi ya damu inayokusanywa kupitia mfumo wa Hospital Transfusion Committee au Hospital Therapeutic Committee. Usimamizi uhusishe pia ngazi zote zinazosimamia huduma za afya ikiwemo kamati za afya za Kijiji, kata, Wilaya hadi Mkoa. Uwepo wa damu salama iwe ni agenda ya kudumu kwenye vikao”. Amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel amesema Ili kukidhi mahitaji ya damu ya nchi, Shirika la Afya Duniani linapendekeza kukusanywa idadi ya chupa za damu ambazo ni sawa na asilimia 1 ya idadi ya wananchi waliopo kwenye nchi au eneo hilo kwa wakati huo.
Kwa nchi ya Tanzania, ikikadiria kuwa tuna wananchi milioni 55, tunatakiwa kukusanya chupa za damu 550,000 ambayo ni sawa na 100% ya mahitaji ya nchi ikilinganishwa na idadi ya wananchi waliopo.
Takwimu za ukusanyaji damu zinaonyesha kuwa na mafanikio ya kuongezeka kwa usukusanyaji damu ambapo Mwaka 2015 jumla ya chupa 104,632 zilikusanywa, kupimwa na kusambazwa. Idadi hii imeongezeka hadi kufikia chupa 309,376 zilizokusanywa mwaka 2019 na chupa 318,514 zilizokusanywa mwaka 2020.
Pamoja na ongezezo hilo, bado lengo la kukusanya chupa 550,000 halijafikiwa ikiwa chupa zilizokusanywa mwaka 2020 (318,514) ni sawa na 60% ya mahitaji ya nchi.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imezindua mradi wa uboreshaji wa huduma za Mama na Mtoto na damu salama Mkoani Dodoma, ikiwa lengo kuu ni kuokoa maisha na kupunguza vifo vya akina Mama vitokanavyo na uzazi pamoja na kupunguza vifo vya Watoto.
Maadhimisho ya siku ya wachangia damu mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Damu ni uhai, Changia damu Maisha yaendelee”.