Na: Hemed Kivuyo
Nimefunzwa Marehemu husemwa kwa mazuri na hasimwangwi.Mola amlaze Pema Joseph Mungai aliyewahi kuwa Waziri wa elimu miaka ya 1996.
Aliyafanya mengi mazuri na kwakuwa ni mwanadamu yapo pia aliyokosea na mojawapo ni hili la kufuta michezo kwenye shule za umma mwanzoni mwa miaka ya 1996.
Zipo taarifa zisizo rasmi kuwa alifuta kutokana na sababu binafsi lakini alama aliyoacha ni kufuta michezo shuleni.
Katika Tangazo hilo ilisema wanafunzi wanahitaji dakika 198 kwa mwaka katika masomo na wanapoteza dakika nyingi kati ya hizo katika michezo.
Lilikuwa ni kosa lililofuta Mazuri mengi aliyofanya. Mungai alizaliwa Oktoba 23-1943 na kuaga Dunia Novemba 8-2016.
Miaka 4 iliyopita Michezo ya Ummiseta iliyopangwa kufanyika Juni 23 hadi juni 22 Jijini Mwanza ilisitishwa na Serikali kwa madai ya kutekeleza agizo la kuongeza madawati Nchi nzima.
Sako kwa bako na hilo hata Umitashumta haikufanyika.
Aliyekuwa Waziri Mwandamizi Mwantumu Mahiza aliwapiga “mkwara” wacheza pool table mkoani Tanga kuwa wanapoteza muda wakazi na waache mara moja.
Michezo shuleni kwa Nchi kama Tanzania ambayo haina vyanzo vya kubaini wanamichezo ni muhimu sana .
Akina John Tegete/Juma Abdull/ Boniface Pawassa/Juma kasseja/Salum Telela/Edibily Lunyamila hawa ni baadhi ya ushahidi wa umuhimu wa michezo shuleni.
Akina Juma Ikangaa/Nyambui/Bay/Saleh Zonga wametokea kwenye michezo.
Lilikuwa ni Kosa kufuta michezo shuleni.nashukuru hata viongozi wajuu huwa wanakiri.
Nirudi kwenye hoja ya Msingi ambayo ni hili la nia ya Wizara ya Habari sanaa utamaduni na Michezo (Serikali) kupendekeza kupunguza idadi ya wachezaji wakigeni (10) kwenye timu za hapa Nchini.
Tuwe wakweli,timu zenye uwezo wakusajili wachezaji wakigeni ni Azam fc/Yanga/Simba Namungo kwa mbalii. Hivyo kama timu hizi zitasajili wachezaji wakigeni wapatao 10 kila timu watakuwa jumla ni 40.
Ama kuna baadhi ya timu ambazo huenda “zinajitutumua” kusajili wachezaji wakigeni ambao hawazidi 4. Tuseme jumla ya wachezaji wakigeni ni 60.
Wachezaji hawa wanalipa kodi,wanakatwa fedha kwaajili ya maendeleo ya soka la vijana zaidi sana wanatoa changamoto kwa wazawa.
Hoja ya wanaosema idadi ya wachezaji wakigeni ipunguzwe ni kuwapa nafasi wachezaji wetu nao kuonekana.
Natafuta neno zuri nadhani nikitumia neno “ni hoja nisiyoiunga mkono” sitokosea. Kwa nini Mchezaji anapata nafasi ya kucheza kwenye timu kama Yanga/Simba na Azam? jibu ni kwasababu Mwalimu ,Kocha amekubaliana na uwezo wake nakatika nafasi anayocheza.
Bila kujali huyu mchezaji niwa Nchi gani. Tunapopunguza idadi nikwamba tunampangia Kocha awapange hawa wazawa hata kama hawana uwezo.
Dunia hii ni pana na milango iwazi kwa wachezani wetu nao kutoka Nje ya Nchi kama akina Msuva/Samata/Himid/Farid /Banda na wengineo.
Nadhani Wizara ingekaa chini na kutafakari kwanini wachezaji wetu hawatoki Nje kucheza soka? na siyo kuwafungia milango wengine wanaotaka kuja kwetu.
Ima wapo wachezani wazawa wanaoonesha jitihada na kuwanyima nafasi wageni “kiufundi” mfano Mohamed Hussein “Zimbwe ” wa Simba alikuwa anachukua nafasi ya kwanza na kumwacha Asante Kwasi benchi.
Ni kwasababu Alionesha uwezo mkubwa na baadaye Simba haikuona haja ya kuendelea kuwanaye.
Kimsingi kufunga milango na kupunguza idadi ya wachezaji wakigeni nikuzidi kufubaza Soka letu ,tutapiga hatua 10 nyuma kama tulivyopiga wakati ule wa Mungai.
Pia kuwa na kanuni/sheria lazima mchezaji anayekuna kucheza soka Tanzania awe amechezea timu ya Taifa lake hii pia ni “hoja nisiyoiunga mkono.”
Siyo kila mchezaji mzuri anapata nafasi ya kuichezea timu Taifa lake. Ni vigumu mchezaji wa timu ya Taifa ya Ghana /Nigeria /Misri/ Algeria/Brazili /Cameroon kuja kucheza soka Tanzania .
Hivyo kuwa na kanuni ya namna hiyo kwenye soka letu ni ngumu. (Labda kuwe na siasa ndani). Mchezaji yeyote mwenye uwezo ataonekana tu kwakuwa soka ni mchezo wa wazi na atapewa nafasi bila kujali katoka wapi.
Tuwaache wageni waje kwetu watoe kodi na changamoto kwa wazawa. Na tuwape shime wa kwetu watoke waende Nje kucheza Soka.
Mh.Waziri Dk.H.Mwakyembe usikubali mazuri uliyofanya yatiwe doa na hili !! Usifanye maamuzi kama ya Mungai. Baadaye wataulizana nani alifanya maamuzi haya? Maamuzi haya yalifanywa chini ya Waziri gani ?
Waziri msomi/Mwanasharia/Mwanahabari/ mtunzi wa Riwaya “Pepo ya mabwege”, endelea kufanya mazuri na kukimbia kwenda mbele, kamwe usirudi nyuma.
Sisi wadau wa michezo tuko nawe, tunakuamini na tunaamini utatuvusha.