Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam imewahukumu watu wawili kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi Milioni moja na Laki tano kila mmoja,kwa makosa mawili ikiwemo kuisababishia hasara Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA zaidi ya shilingi milioni 267.
Watu hao ni Mhandisi Baraka Mtunga (43) na Rajabu Thabiti (42) ambao wamesomewa hukumu hiyo hii leo na Hakimu Mkazi Mkuu Kassian Matembele ambapo upande wa mashtaka uliowakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine na wale wote wanaofikiria kufanya kitendo kama hicho.
Oktoba 16,mwaka huu washtakiwa hao waliandika barua kwa Mkurugenzi wa mashtaka kuomba kufanya Makubaliano ya kukiri kosa hilo ambapo baada ya makubaliano hayo wametakiwa kulipa shilingi za Kitanzania milioni 267,656,794.30 Kama fidia ambapo tayari wamelipa milioni 200 na kiasi kilichobaki kitalipwa ndani ya miezi sita.
Kwa mujibu wa hati ya Mashtaka washtakiwa wote kwa pamoja katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani katika kijiji cha Kanjoo Wilaya ya Bagamoyo walisimika na kuvitumia vifaa vya kieletroniki bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Katika shtaka jingine kati ya Desemba 13,2019 na Septemba 28,2020 waliisababishia hasara Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA ), shilingi za Kitanzania milioni 267,656,794.30.