Kamati Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu.
Taarifa ya TFF leo imesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013.
Maamuzi hayo yamechukuliwa baada ya kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana ambapo pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya TFF.
Wambura alifikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
Kamati ya Maadili imepokea malalamiko yanayomuhusu Wambura ikiwa ni uvunjifu wa kanuni za Maadili Tolea la 2013 na Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015.
Wito huo umemtaka Wambura kufika mbele ya Kamati ya Maadili baadaye leo na ana hiyari ya kufika kutoa utetezi huo kwa njia ya mdomo, kutuma kwa maandishi, kuleta mashahidi au kutuma muwakilishi akiambatana na barua ya uwakilishi.
Makosa aliyoshtakiwa Wambura ni;
1.Kupokea/Kuchukuwa fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanui za Maadili za TFF Toleo la 2013
- Kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEM LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013
- Kufanya Vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (Kama ilivyorekebishwa 2015).
Akizungumzia hatua hiyo, Wambura amesema kwamba Kamati iliyomfungia haina mamlaka, kwa sababu yeye anawajibika kwenye Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu.
Wambura amesema kwamba kwa sasa anasubiri barua rasmi kutoka kwenye Kamati hiyo ili kuchukua hatua rasmi.