Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro, Agnes Mkandya amemwaga machozi alipokuwa akiulizwa maswali na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Tukio hilo lilitokea jana wilayani humo baada ya kamati hiyo kumuuliza Mkurugenzi huyo maswali mbalimbali ikiwa ni pamoja na udanganyifu na ubadhirifu wa fedha mkubwa unaoonekana kufanywa na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo.

Swali lililomliza Mkurugenzi huyo liliulizwa na Mbunge wa viti maalum, Leah Komanya (CCM), aliyetaka majibu kuhusu wizi wa mapato kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia karatasi maalum, unaofanywa na watendaji hao.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo ubadhirifu mkubwa wa fedha ndani ya Halmashauri hiyo na kueleza hatua alizochukua, huku akijitetea kuwa yeye ni mgeni hivyo mambo mengi bado hajayafanyia kazi.

“Kamati ielewe kwanza Halmashauri ya Gairo imeoza na ni chafu kwa sababu kuna ubadhirifu mkubwa. Tayari nimewasimamisha kazi watumishi tisa wa idara, lakini kumbukeni na mimi ni mgeni sina muda mrefu,” alijibu Mkurugenzi huyo kabla ya kuanza kumwaga chozi.

Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake, Vedastus Ngombale Mwiru walimtuliza kwa kumbembeleza wakimtaka aondoe woga kwani ni maswali ya kawaida aliyoulizwa.

Baada ya hali hiyo, Mwenyekiti huyo aliamuru majibu ya maswali hayo na mengine kutolewa na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo kwakuwa yeye alikuwepo muda mrefu.

Dk. Tulia afunguka, asema Ukawa walimtukana tusi kubwa
Polisi wawabana Original Comedy kwa kuvaa mavazi ya ‘Kipolisi’ harusini