Siku chache baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza kuwa anapanga kukaa chini na wabunge wa vyama vya upinzani kutafuta namna ya kuondoa tofauti ndani ya Bunge hilo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amefunguka kuhusu mgogoro wake na wabunge wa Ukawa.

Dk. Tulia amesema kuwa anawashangaa wabunge hao kudai kuwa anawaonea na kwamba sababu ni kutokuwa na uzoefu wa kuliongoza Bunge hilo. Alisema kuwa kuliongoza Bunge ni kutumia kanuni na sio uzoefu kwahiyo mtu yeyote anayeweza kuzisoma na kuzielewa kanuni zile anaweza kuongoza Bunge.

“Nashangaa wengine wanasema kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu. Unajua zile kanuni hata ukipewa wewe, ukishazielewa vizuri hazihitaji uzoefu wowote. Kulalamika kuwa nawapendelea ni jambo la kawaida,” Dk. Tulia anakaririwa na Mtanzania.

Akifafanua hoja yake, Dk. Tulia alitolea mfano wa siku ambayo wabunge wa Ukawa walitoka nje wakipinga Bunge kutorushwa ‘Live’, akieleza kuwa aliyekuwa anaongoza kikao hicho alikuwa Mwenyekiti wa Bunge ambaye ni mzoefu.

Akizungumzia kauli ya Spika wa Bunge kuwa kuongoza Bunge la 11 lenye wabunge wengi wapya kunahitaji uvumilivu, Dk. Tulia alisema kuwa asingependa kuzungumzia kauli ya Spika, lakini alikuwa mvumilivu pia.

Alisema kuwa alitukanwa tusi kubwa wakati Wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa kwenye umoja wa wanawake Bungeni, alitukanwa tusi kubwa lakini alikaa kimya akavumilia.

“Ungeona Hansard tusi walilonitukana… lakini ulisikia nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? Wao wanaongea vibaya… watukane, mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.

Alisema kuwa malalamiko ya wabunge wa Ukawa kuwa anapendelea upande mmoja na kuitetea Serikali ni jambo la Kawaida.

Akamatwa kwa kuwapa ombaomba maandazi yenye sumu nje ya Msikiti
Mkurugenzi amwaga machozi mbele ya Kamati ya Bunge