Waziri wa nchi ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, ametoa wito kwa wanafunzi waliokosa nafasi za kujiunga na masomo ya kidato cha tano kwa kukosa tahasusi zinazokidhi vigezo kuomba nafasi za masomo katika vyuo vinavyosimamiwa na NACTE ili kuweza kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika vyuo hivyo.
Jafo ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu matokeo ya uchaguzi wa awamu ya pili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.
“Wanafunzi waliochaguliwa wote wanatakiwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano awamu ya pili kuhakikisha wanafika shuleni kuanzia Septemba 6 hadi 20 mwaka huu ambapo mwanafunzi atakeyeshindwa atakuwa amepoteza nafasi yake”, amesisitiza Jafo.
Aidha Jafo amesema kuwa jumla ya wanafunzi 1,017sawa na asilimia 11.82 wamekosa tahasusi zinazokidhi vigezo na kwa sababu hiyo hawajachaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika awamu ya pili.
Jafo ameeleza kuwa kuwa wanafunzi 7,586 kati ya 8,603 walikosa nafasi awamu ya kwanza wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika awamu ya pili.