Wakati nyota kutoka nchini Ivory Coast Ibrahima Fofana, akianza majaribio leo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imempokea straika mwingine raia wa Niger, Mossi Moussa Issa.

Issa, 22, ametua nchini usiku wa kuamkia leo na ataanza rasmi majaribio kesho Jumamosi akiungana na Fofana, ambao wote wanawania nafasi ya kusajiliwa na mabingwa hao kwa ajili ya msimu ujao.

Straika huyo ametokea timu ya Sahel Sporting ya Niger, alikofunga mabao manne ndani ya mechi nane alizocheza pia amewahi kucheza kwa mabingwa wa Morocco FUS Rabat mwaka 2013 na AS Douanes (Niger).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kufika makao makuu ya Azam Complex, Chamazi na Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba, Issa alisema amefarijika sana kupata nafasi ya kuja Azam FC kuonyesha kipaji huku akidai kuwa amejipanga kupambana ili kusajiliwa na timu hiyo.

“Nimejiandaa vizuri na nipo asilimia 100 kupambana kupata nafasi hiyo ya kusajiliwa,” alisema kwa ufupi Issa.

 

Zeben anena

Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema kuwa anatarajia kumwangalia mchezaji huyo kwenye mazoezi ya kesho Jumamosi baada ya leo kuanza kumtazama Fofana.

“Leo nimeanza kumwangalia mchezaji aliyefika juzi (Fofana), kesho nitamwona pia mchezaji mwingine (Issa), nitawaangalia kwa kipindi kifupi kilichobakia na hapo ndipo nitakuja na maamuzi ya mwisho,” alisema.

Katika hatua nyingine kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Ashanti United Jumapili ijayo, anatarajia kutoa hatima ya makipa wawili Mghana Daniel Yeboah na Mhispania Juan Jesus Gonzalez waliokuwa kwenye majaribio ya kujiunga na Azam FC wakiwania nafasi moja ya usajili wa golikipa.

 

Mechi mbili za kirafiki

Akizungumzia mechi za kirafiki itakazocheza Azam FC, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema kuwa timu hiyo itaanza kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki keshokutwa Jumapili saa 3 asubuhi dhidi ya Ashanti United kabla ya kuvaana na timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) Jumatano Ijayo.

Chanzo; Azam FC

Daktari Wa Azam FC Atua Nchini
TFF Yawakumbusha Waliopendekezwa Tuzo Za VPL 2015-16