Katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 2022, Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, imezindua zoezi la kupanda miti katika Halmashauri zake mbili, Nsimbo na Manispaa ya Mpanda) ambapo jumla ya miche zaidi ya milioni 3.5 inatarajiwa kupandwa msimu huu.
Akizindua zoezi hilo lililofanyika katika shule ya Sekondari Nsimbo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Leah Gawaza, amesema zoezi hilo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya uhifadhi wa mazingira.
Amesema, kutokana na shughuli za kibinadamu yapo baadhi ya maeneo miti imepungua hivyo namna pekee ya kuirejesha ni kuhamasisha wananchi, taasisi mbalimbali za uhifadhi wa mazingira kushiriki zoezi hilo.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Nsimbo, Mohammed Ramadhani amesema lengo la zoezi hilo ni kuhamasisha jamii kuendelea kutunza mazingira ili kuzuia athari hasi za mabadiliko ya tabia ya nchi zinazosabbishwa na kutokuwepo kwa miti ya kutosha.
Awali, zoezi kama hilo lilifanyika katika eneo inakojengwa shule ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Mpanda Pre & English Medium School, iliyopo kata ya Misunkumilo mjini Mpanda ambapo Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli aliwaongoza watumishi na wananchi wake katika zoezi la kupanda miti.