Bohari ya Dawa (MSD), imepongezwa kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vilivyokabidhiwa katika vituo vya afya mkoani Tanga.
Akizungumza leo Julai 17,2022 Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makorora mkoani Tanga, Dkt. Angelina Meshack amesema walipokea vifaa vya chumba cha upasuaji ikiwemo kitanda cha upasuaji, mashine ya dawa ya usingizi na taa zinazotumika wakati wa upasuaji.
“Tulikuwa hatufanyi upasuaji kabisa kwa hiyo tulivyopokea fedha kwa ajili ya ukarabati majengo ya kufanyia upasuaji tulifanya hivyo na baadae vifaa vililetwa na MSD na kuanza kutoa huduma za upasuaji,”amesema Dkt. Meshack.
Amesema, baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo walianza kutoa huduma ya upasuaji kwa akinamama wajawazito na upasuaji mdogo tofauti na hapo awali ambapo wagonjwa walipelekwa Hospitali ya Bombo.
“Ujio wa vifaa hivi umemrahisishia mama mjamzito, akipata changamoto tunaweza kumpa huduma ya upasuaji na tunaokoa maisha ya mama pamoja na mtoto,” amebainisha Dkt. Angelina.
Hata hivyo amesema, hali ya upatikanaji wa tiba katika kituo hicho ni nzuri kutokana na dawa muhimu kupatikana kwa asilimia 90 na wanaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kituoni hapo.
Kwa upande wake Mfamasia wa Kituo cha Afya Ngamiani, Michael Mrosso amesema walipokea vifaa tiba kwa aajili upasuaji pamoja na jenerata, ambavyo vilikuwa ni kilio chao cha muda mrefu.