Serikali ya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutafuta suluhu za kimaendeleo na kudai kuwa huenda mambo yasieleweke kwasasa lakini yatakuja kueleweka mbele ya safari.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi hii leo Julai 14, 2022, katika Kongamano la kumkumbuka aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin William Mkapa linalofanyika katika Hotel ya Golden Tulip Visiwani Zanzibar.
Amesema, anamkumbuka Hayati Mkapa kwa mambo mengi ikiwemo falsafa na wosia alioucha kuhusu ujasiri na changamoto za kufanya mageuzi pale inapohitajika kwa maslahi mapana ya taifa bila kuhofia.
“Katika kitabu chake alizungumzia ugumu alioupata katika kufanya ubinafsishaji, Mkapa aanasema kuwa kiongozi kunahitaji utayari na kubadilika, ikiwemo kuendana na mawazo mapya na ujasiri wa kutekeleza yaliyo sahihi,” amesema Rais Mwinyi.
Ameongeza kuwa, maa na halisi ya uongozi pia inajidhihirisha kwa muasisi wa Mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume ambaye aliwahi kusema ni heri kugombana na mtu katika jambo utakalokuja kupatana baadaye.
Aidha, Rais Mwinyi amefafanua kuwa mageuzi kama yalivyo mapinduzi, huja na mafanikio bila kukosekana kwa changamoto kudai hiyo ni tabia ya wanadamu kupenda kushikilia jambo alilolizoea hata kama lina madhara.
“Wahenga walisema mazoea yana tabu, binadamu angependa yale mabadiliko tu ambayo hayaji na changamoto ama hayaharibu mazoea yake lakini kwa bahati mbaya mawili haya hayawezi kutenganishwa,” amesisitiza Dkt. Hussein Mwinyi.
“Kwa kulitambua hilo serikali imedhamiria kushirikisha sekta binafsi katika nyanja zote za maenedeleo sababu ni jambo sahihi kufanya hivyo,”amesema Rais Mwinyi.
Hata hivyo, ameahidi kuendelea kuwaelemishwa wale wote wenye mashaka na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika shughuli za kimaendeleo na kusema Serikali yake imedhamiria kwa kuwa ni sahihi kufanya hivyo.
“Wale ambao wanapata ugumu kutuelewa, fikra na matendo yetu watakuja kuyaelewa matokeo watakapoyaona na huo ndio ustahimilivu na ushupavu wa uongozi aliouzungumzia Hayati Benjamin Mkapa na viongozi waliotutangulia,” amebainisha Rais.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa, akiwemo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Hayati Benjamin William Mkapa, alizaliwa katika familia ya Mzee William Matwani na Mama Stephania Nambaga Novemba 12, 1938, katika kijiji cha Lupaso, Masasi, mkoani Mtwara na alifariki dunia Julai 24, 2020 akiwa na umri wa miaka 81.