Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema utaratibu wa ajira mpya za walimu unaelekeza kuwa, ili kuajiriwa ni lazima muhusika afanye mtihani na ufaulu wake utampa sifa ya kushiriki usaili kwa minajili ya kupata kazi.
Prof. Mkenda ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo za walimu na kuongeza kuwa ajira ya ualimu inahusisha utumaji wa maombi katika tovuti maalum ya maombi ya ajira, na atakayepata nafasi hufanyiwa usaili kisha kupangiwa eneo la kazi.
Amesema, “hakutakuwa na vimemo wala ‘connection’ hatutaangalia ni mtoto wa nani, na mbali na mitihani watafanya ‘interview’ vile vile kama kawaida, tunataka iwe kama udaktari tu maana ubora wa elimu bila walimu bora ni kazi bure.”
Katika hafla hiyo, shindano liliwalenga walimu wa awali na msingi wanaofundisha kuhesabu na hisabati vikiwemo vipengele vya Geometri, Aljebra, namba kamili na takwimu ambapo umahiri wa matumizi ya teknolojia, mawasiliano mazuri na wanafunzi, mbinu za kushawishi wanafunzi kupenda somo, ni miongoni mwa vigezo vilivyoangaliwa.