Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Kamati za ulinzi wa Mwanamke na Mtoto kwenye mtaa zijipange kujua na kufumbua maovu yanayotendeka katika jamii kwani vitendo vya ukatili vingi vinatokea katika ngazi ya familia na havigunduluwi mpaka malanga yatokee.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Aprili 16, 2022 alipotembelea familia ya mtoto miaka miwili na miezi minne, aliyefahamika kwa Jina la Mage, aliyedaiwa kuuawa kikatili na mama yake mkubwa aitwaye Latifa Bakari (33) mkazi wa Mabibo mkoani Dar es salaam.

Waziri Dkt. Dorothy Gwajima

Dkt. Gwajima amezitaka Mamlaka za Serikali za mitaa na Kata kuhakikishe zinafuata mwongozo wa uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ili kupunguza matukio ya ukatili kwa watoto nchini.

“Inasikitisha huyu mtoto alikuwa anaonyesha wazi namna ambavyo hana amani hapa anapoishi, lakini Mjumbe wa Shina aliambiwa hakulichukulia hatua mpaka mtoto ameuawa, naagiza nchi nzima ngazi za Serikali za mitaa na Kata anzisheni klabu za kukutana na watoto watasema wanayoyapitia,” alisisitiza Dkt. Gwajima

Aidha Waziri Dkt. Gwajima ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wanatoa taarifa kabla ya kuchukua hatua na kwa wazazi ambao wameshindwa malezi ya watoto watoe taarifa kwa maafisa Ustawi wa Jamii kuliko kuua, kutelekeza au kupiga kupita kiasi watoto.

“Tunao watoto wanaokimbilia mitaani, kabla hujabariki hilo tunaomba uchukue jukumu lako kukumbuka kwamba Rais ameiunda Wizara hii na wapo maafisa wa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kwenye Kata mnachotakiwa kufanya mpelekee huko waambie wao wanaweza kufanya upembuzi yakinifu wa tatizo lako.” alisema Dkt. Gwajima.

Hata hvyo Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa anataka kuona Sheria ikichukua mkondo wake na mtuhumiwa akifikishwa mahakamani ili haki itendeke.

“Mlishindwa kujadili kindugu wakati mtoto anateswa kwa sasa Wizara tutaifuatilia hatutaki kuona watu wanafanya ukatili kwa wanawake na watoto mpaka wanafikia hatua ya kuua kabisa, halafu mnataka kukaa kifamilia tutawatetea watoto kwa ustawi wao, wazee na wanawake.” alisema Waziri Gwajima.

Akisimulia kisa hicho, Mkazi wa Mabibo Kisimani, Furaha Pius amesema mtoto alikuwa na alama nyingi za vipigo na alishawahi kumwambia Mjumbe wa Shina kuhusu suala hilo ili aweze kuchukua hatua au kutoa taarifa sehemu husika dhidi ya kitendo hicho.

Kwa Upande wake Mama Mkubwa wa mtoto huyo, Mariam Damas alisema majirani wamesema kwamba mtoto huyo alikuwa akipigwa kila siku kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukojoa kitandani.

“Sio sahihi kumpiga mtoto huyo kwa kiasi hicho cha kinyama, vitendo hivi lazima vikomeshwe.Lakini suala la mama yake kumleta mtoto huku sisi hatukuliafiki na wakati tunataka kuchukua hatua haya yakatokea,” alisema Mariam

“Tunaiomba Serikali ichukue hatua kwa sababu mume wa mtuhumiwa anataka kumwekea dhamana mkewe atoke, sisi tunaomba tena sana haki itendeke maana wameshaanza kutaka limalizwe kifamilia.” alisisitiza Mariam

Wafahamu Maharamia/Vibaka wa Soweto (ORLANDO PIRATES)
Habari kubwa kwenye magazeti leo, April 17, 2022