Rais Yoweri Museveni amesema kuwa serikali yake iliamua kumkamata Dk. Besigye na kumshikilia nyumbani kwake ili kuzuia vurugu baada ya zoezi la kupiga kura na kutangaza matokeo.

Akiongea na BBC leo asubuhi, Rais Museveni ameeleza kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Dk. Besigye alipanga kutangaza matokeo yake mwenyewe mbayo sio ya kweli na kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, vitendo ambavyo havikubaliki.

“Walikuwa wanataka kufanya fujo. Kwanza walikuwa wanataka kutangaza matokeo yao wenyewe ya uongo. Pili walitaka kufanya fujo za kuharibu mali,” alisema Museveni.

Alisema kwakuwa tayari uchaguzi umemalizika na matokeo yametangazwa na Tume ya Uchaguzi yaliyompa yeye ushindi wa kishindo, atamuachia huru Dk. Besigye ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu.

Kadhalika, Museveni alieleza kuwa serikali yake haina mpango wa kuweka ukomo wa Urais nchini humo kwakuwa tayari Bunge liliona ni vyema kuwa na kipindi kisichokuwa na ukomo. Hata hivyo, alisema kuwa hana mpango wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ili aendelee kubakia madarakani.

“Hakuna mpango wowote. Hatujazungumzia hilo. Lilikuja kwenye baraza la mawaziri tukasema hapana, hakuna haja ya kuongeza,”Museveni anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Museveni ambaye anaiongoza Uganda tangu mwaka 1986, amepinga ripoti za waangalizi zilizodai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Amesema kuwa wanaotoa madai hayo kwa madai kuwa nguvu ya jeshi ilitumika zaidi hawaijui siasa ya Uganda kwani wanasiasa wengi hawajakomaa kisiasa hivyo wanaweza kuanzisha fujo muda wowote.

 

Exclusive: MC Pilipili asimulia alivyotafutwa na TRA baada ya kutangaza Ma-MC walipe kodi, Utacheka (Audio)
Meya wa Kinondoni avutana na makonda