Lydia Molell, Kilosa – Morogoro.
Zaidi ya kaya 100 zimekosa makazi baada ya Nyumba zao kusombwa na kubomolewa na Maji, kufuatia Mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia leo Desemba 10, 2023 ambazo pia zimeharibu madaraja manne Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Kilosa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewapa pole waathiriwa huku akiwataka kuacha kujenga katika maeneo ambayo Mkondo wa maji unapita, ili kuepuka adha zinazosababishwa na maafuriko.
Amesema, tayari Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya imeanza kufanya tathmini ya athari iliyotokea na itakapomilika misaada mbalimbali itatolewa, ili kuwasaidia Wananchi walioathirika na mafuruko hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema Madaraja yaliyosombwa na maji yamekwamisha shughuli za kijamii, kwani mawasiliano kati ya Morogoro – Kilosa mjini yamekatika kufuatia Daraja lililojengwa kwa muda ya Ilonga kusombwa na maji.
Aidha, Shaka pia amewataka Wananchi waishio kando za mito kuhama mara moja katika maeneo hayo, kwani Mvua hazitabariki na uwepo wa Maji Kilosa hautegemei Mvua bali hukusanyika kutoka katika maeneo tofauti.
Nao baadhi ya Wananchi walioathirika na Maafuriko hayo, wamesema hawajajenga katika mikondo ya maji bali ujenzi wa daraja la mwendokasi umesababisha maji kukosa muelekeo na kuingia katika maeneo yao.