Safu ya ulinzi imeshikilia hatma ya Taifa Stars katika mchezo wake muhimu wa mwisho wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 ugenini dhidi ya Algeria, keshokutwa Alhamis (Septemba 07).

Katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi E, utakaochezwa kuanzia saa 4:00 kwenye Uwanja wa Mei 19, 1956 jijini Annaba, Taifa Stars inayoshika nafasi ya pili inahitaji ushindi au sare ili kujihakikishia nafasi ya kwenda AFCON, nchini Ivory Coast, mwakani.

Kumbukumbu ya mechi tano zilizopita baina ya timu hizo mbili ambazo zilichezwa Algeria inaonyesha safu ya ulinzi imekuwa na takwimu za kuruhusu wastani wa mabao matatu katika kila mchezo.

Algeria imekutana na Taifa Stars mara tano ikiwa nyumbani na imeibuka na ushindi mara tatu na zimetoka sare mara mbili.

Katika mara hizo tano za mashindano tofauti, Algeria imefunga bao katika kila mchezo ikiizidi kidogo Taifa Stars ambayo ilifanya hivyo katika michezo minne.

Mara ya kwanza kwa Taifa Stars kucheza katika ardhi ya Algeria ilikuwa 1995 na kupoteza kwa mabao 2-1, mechi ya kufuzu fainali za AFCON na kisha 2002 ikalazimisha sare ya 1-1 katika mechi ya kimataifa ya kirafiki.

Kipa wa zamani wa Taifa Stars, Juma Pondamali amesema matokeo ya nyuma yasiwatishe wachezaji wa timu hiyo dhidi ya Algeria.

“Ulinzi ni suala la timu nzima. Inawezekana mabeki wakacheza vizuri, lakini kama hawatopata sapoti ya timu nzima wataishia kulaumiwa tu. Timu inatakiwa ishambulie na kuzuia kwa pamoja, lengo litafanikiwa.

“Wakicheza kitimu uwezekano wa kuwafunga au kupata sare dhidi ya wale Algeria upo. Maana wale hawana cha kupoteza hivyo hawatotumia nguvu kubwa,” amesema Pondamali.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 6, 2023
Mike Dean amaliza utata Penati ya Arsenal