Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju amezungumzia suala la wakuu wa mikoa kutoa matamko ya kusitisha likizo za watumishi wa umma kwa kuwataka wafanye kazi tu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na kituo cha runinga cha Azam, Masaju amesema amekuwa akisikia kupitia vyombo vya habari kuhusu taarifa za kuwepo matamko hayo kutoka kwa baadhi ya wakuu wa mikoa.

Alisema kuwa hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria na kwamba sheria na katiba ya nchi lazima ifuatwe na watu wote nchini bila kujali cheo cha mtu aliyetoa matamko hayo.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kuwa hajawahi kupokea malalamiko yoyote ofisini kwake kutokana na matamko hayo ambayo amekuwa akiyasikia kwenye vyombo vya habari pekee lakini hajapata taarifa rasmi.

Aidha, alikataa kueleza moja kwa moja kama uamuzi huo unaochukuliwa na baadhi ya wakuu wa mkoa ni kosa kisheria.

“Mimi sio Jaji wa kusema kuwa waliosema hivyo wamevunja sheria, lakini nataka kusema kuwa sisi sote tunaongozwa na sheria na katiba ambavyo lazima vifuatwe.”

Kumekuwepo na taarifa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla walitangaza kusitisha likizo kwa watumishi katika mikoa hiyo kwa sababu za kuwataka wafanye kazi tu!

Kwa mujibu wa sheria, likizo ni haki ya mfanyakazi.

Hitz Fm Ya Zanzibar Yachomwa Moto, Mtangazaji Asimulia Alivyonusurika Kukatwa Shingo
Magufuli Atoa Siri Ya Kwanini Anaweza ‘Kutumbua Majipu’ Bila Kujali Jina