Mwanasheria wa rapa Meek Mill amemshambulia vikali Jaji aliyemhukumu mteja wake huyo kifungo cha miaka 2-4 jela.

Joe Tacopina, ambaye ni mmoja kati ya wanasheria wanaomtetea Meek Mill amedai kuwa Jaji huyo alitoa hukumu akiwa na kinyongo kwani alikuwa anataka Meek Mill aachane na dili la lebo ya Roc Nation na kujiunga na lebo ya rafiki yake.

Mwanasheria huyo alienda mbali zaidi akidai kuwa Jaji huyo mwanamke alikuwa na kiu ya kutaka kutajwa kwenye wimbo mmojawapo wa rapa huyo, hivyo kutopata nafasi hiyo kuliongeza hasira zake.

Akisoma hukumu iliyompeleka Jela Meek Mill, Jaji huyo alieleza kuwa amemvumilia tangu mwaka 2009 alipokuwa na kesi ya kumiliki silaha kinyume cha sheria na dawa za kulevya.

Naye Jay Z alionesha hasira zake juu ya hukumu hiyo akidai Meek amekuwa kwenye kipindi cha uangalizi maalum (probation) kwa muda mrefu, ambao ni miaka 11.

“Meek alifunguliwa kesi alipokuwa na miaka 19. Hivi sasa ana umri wa miaka 30. Bado yuko kwenye kipindi cha uangalizi maalum, miaka 11. Jaji amevunja. Kweli anapaswa kwenda jela miaka 2-4 kwa sababu tu alikamatwa akikimbiza pikipiki?!” Ni tafsiri isiyo rasmi ya sehemu ya maelezo ya Jay Z.

Tayari Meek ameshakamilisha taratibu za kuanza kifungo chake, ingawa taarifa zinaeleza kuwa gereza ambalo atatumikia kifungo hicho litakuwa siri kwa ajili ya usalama wake.

Hata hivyo, wanasheria wake wameweka wazi dhamira ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

RPC Kagera azungumzia chanzo cha mlipuko wa bomu
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 9, 2017