Mahakama ya nchini Somalia, imemhukumu Mwandishi wa Habari wa kujitegemea kifungo cha miezi miwili jela, kwa tuhuma za kutishia usalama wa taifa katika kesi ambayo imekuwa ikikosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu na makundi ya wadau habari.
Rais wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Somalia (SJS), Ibrahim kupitia ukurasa wake Twitter ameandika kuwa, “Kuhukumiwa kwa Abdalle Ahmed Mumin ni ukiukaji wa wazi wa haki, hivyo tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huo dhidi na dhidi ya mwanahabari huyu, ambaye ni katibu mkuu wa SJS.”
Kabla ya hukumu, mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwemo Amnesty International, Human Rights Watch na Taasisi ya Kimataifa ya Vyombo vya Habari, yalitoa wito wa kufutwa kwa mashtaka hayo, yakisema kwamba Mumin amekuwa akikabiliwa na vitisho na mateso yanayoendelea kutoka kwa mamlaka ya Somalia kwa kutetea haki ya uhuru wa kujieleza.
Abdalle Ahmed Mumin alikamatwa mwezi Oktoba, muda mfupi baada ya uamuzi wa serikali kuongeza ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari, ambavyo mamlaka inaamini vinahusika katika propaganda kwa waislamu wenye itikadi kali Shebab.