Mzozo kati ya Serikali za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), unaendelea kushika kasi huku Rais wa Kongo akiongoza Baraza Kuu la Ulinzi kupata majibu ya kwanini Warwanda wanaleta uchokozi.
Waziri wa Mawasiliano na Msemaji wa Serikali, Patrick Muyaya amesema baaada ya mkutano huo, serikali ilisema ilifikiria kusitisha mikataba yote iliyokubaliana na nchi hiyo jirani yake, ikimtuhumu kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23.
“Baraza la Juu la Ulinzi limechukua hatua zifuatazo, kwanza, wanaitaka Rwanda kuwaondoa mara moja wanajeshi wake wanaofanya kazi chini ya usiri wa kundi la kigaidi la M23, kutoka eneo la Kongo,” amesema Muyaya.
Katika hatua ya pili Waziri Muyaya amesema wanaiomba Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo isitishe kazi, itifaki zote za makubaliano na mikataba iliyohitimishwa na Rwanda hivi Karibuni.
Maendeleo mapya ya mgogoro huo, yanakuja baada ya maandamano kadhaa dhidi ya Rwanda kufanyika katika miji tofauti ya Kongo ambapo Jumatatu wiki hii Juni 13, 2022 mji wa mpakani wa Bunagana, ulitekwa na waasi na kuwalazimu maelfu ya wakazi kukimbia.
Rwanda na Uganda, zimekanusha kwa miaka mingi shutuma zilizopo za kuunga mkono kundi la M23, huku Serikali ya Rwanda ikivilaumu vikosi vya Kongo kwa kuwajeruhi raia kadhaa katika mashambulizi baada ya kuvuka mpaka.
Kundi la M23, lilipata umaarufu takriban muongo mmoja uliopita wakati wapiganaji wake walipoiteka Goma, jiji kubwa zaidi mashariki mwa DRC ambalo liko kando ya mpaka na Rwanda.
Hata hivyo, waasi hao walifukuzwa kutoka Goma na baada ya makubaliano ya amani, wapiganaji wengi wa M23 walijumuishwa katika jeshi la Taifa la DRC na mapema mwaka huu waasi hao walirejea, na kuanzisha mashambulizi dhidi ya jeshi la DRCongo baada ya kusema serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake za muongo mmoja.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyata alitoa wito kwa Kikosi kipya cha Kanda ya Afrika Mashariki kilichoanzishwa kuchukua hatua ya kulinda usala huku wakifanya jitihada za kuleta mapatano baina ya pande hizo mbili zenye mzozo uliotawala eneo la mashariki mwa DRCongo.