Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nasreddine Nabi amesema hana budi kutumia muda uliobaki kurekebisha makosa alioyaona kwenye kikosi chake, ili wakamilishe lengo la kuibuka na ushindi dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal.

Young Africans itakuwa mwenyeji wa Al Hilal Jumamosi (Oktoba 08) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda Khartoum-Sudan kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili mwishoni mwa juma lijalo.

Kocha Nabi amekiri kuwa wachezaji wake walicheza kwa kiwango cha kawaida juzi Jumatatu (Oktoba 03) dhidi ya Ruvu Shooting licha ya kuibuka na ushindi wa 2-1, halia mbayo inamlazimu kufanya maboresho na marekebisho mapema, kabla ya kuivaa Al Hilal.

Amesema anatumia muda uliosalia kufanya marekebisho na maboresho kwenye kikosi chake huku akitoa msisitizo kwa kila mchezaji kuhakikisha anapambana kwa nafasi yake ili kufikia lengo la kuwa tayari kuelekea mchezo dhidi ya Al Hilal.

“Hatujafanya vizuri sana katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, nikiri wachezaji wangu hawakucheza katika kiwango kilichozoeleka, hata hivyo muhimu tulipata alama tatu.”

“Makosa bado yapo tuna siku kadhaa zimebaki kuelekea katika mchezo wetu dhidi ya Al Hilal, nitahakikisha ninazitumia siku hizi kurekebisha mapungufu niliyoyaona ili tukafanye vizuri Jumamosi (Oktoba 08).”

“Kila mmoja katika kikosi changu anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Al Hilal, sitakuwa tayari kuruhusu makosa ambayo yatafanya tuwe katika nafasi ngumu, kila mmoja anapaswa kufahamu hilo.” amesema Kocha Nabi

Mshindi wa jumla wa mchezo huo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, atatinga hatua ya Makundi ya Michuano hiyo.

Mwongozo watolewa utafiti magonjwa ya akili
Mbwana Samatta achomoza kikosi bora Afrika