Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameahidi kulegeza uzi wa kubana wasanii na kazi zao baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wadau.

Nape ametoa ahadi hiyo jana katika tuzo za kituo cha runinga cha ‘East Africa TV’ (EATV Awards 2016), ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Alisema kuwa Serikali itaendelea kubana katika sekta nyingine kama inavyofanya, lakini italiangalia kwa jicho la tofauti sekta ya sanaa ili ‘mambo yaende sawa’.

“Na mimi nimepita mtaani naambiwa ‘Nape mmebana sana.’ Wakati mwingine tunataka kufanya mambo tunaambiwa tumepitiliza. Wakati mwingine tutafumba jicho moja watu wapitilize kidogo ili mambo yaende sawa sawa,” alisema Waziri Nape.

Nape ametoa kauli hiyo wakati ambapo Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limekuwa likilaumiwa na wasanii kwa kufungia kazi zao na kuwapa adhabu kali kwa kukiuka maadili, hatua wanayodai imekuwa ikiwaingiza hasara.

BASATA wameendelea kuahidi kuwanyoosha wasanii ili wazingatie maadili katika kazi zao, japo katika siku za hivi karibuni kuna baadhi ya video za nyimbo za bongo fleva ambazo zimeonekana kufumbiwa jicho moja ili zipite kama alivyosema Waziri Nape.

Wasira: Sijateuliwa kuwa msemaji wa CCM
Masauni: Tutazishughulikia Asasi zote za kiraia zinazotetea ushoga