Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi amesema ataendelea kuwa mkali kwa wachezaji wake katika suala la nidhamu kwa msimu wa 2022/23, ili kufanikisha malengo ya kutetea Ubingwa na kufanya vizuri Kimataifa.

Young Africans itaanza rasmi kambi leo Alhamis (Julai 21), baada ya wachezaji kuwasili kambini hapo kuanzia jana Jumatano (Julai 20), tayari kwa maandalizi ya msimu mpya ambao rasmi utafunguliwa Agiosti 13 kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC.

Kocha Nabi amesema anaamini silaha kubwa ambayo inapaswa kutumika kwa wachezaji wake ni Nidhamu, hivyo kila wakati na kila watakapokwenda wanapaswa kuitumia ili kufanikisha mipango waliojiwekea.

“Siku zote nimekua naamini katika nidhamu kwa wachezaji, kila mmoja akijiheshimu na kuheshimu misingi ya timu, ninaamini tutafanikiwa, hivyo ndivyo Young Africans ninataka iwe,”

“Kama wachezaji watashindwa kujiheshimu na kutambua thamani ya klabu hii, itakua vigumu kwetu kutetea Ubingwa wa Mataji tulioyachukua msimu wa 2021/22, hivyo silaha ya kwanza kuyalinda mataji yetu ni kila mmoja wetu kuwa na nidhamu.”

“Msimu ujao utakua mgumu sana kwetu, kwa sababu timu pinzani zinajiandaa na zitahitaji kucheza vizuri zaidi yetu, zitahitaji kuvunja mwiko wetu wa kutopoteza mchezo ambao tunaendelea nao hadi sasa, kwa hiyo ni jukumu letu sote kulitambua hilo kwa kuhimizana ili kuendelea kufanya vizuri.” Amesema Kocha huyo kutoka nchini Tunisia

Kabla ya kuanza msimu wa 2022/23, Young Africans itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki katika Siku ya Wananchi (Agosti 06) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC, Vipers SC zamaliza sakata la Manzoki
Abdul Sopu afunguka alivyozikataa Simba SC, Young Africans