Bondia wa Tanzania Nasibu Ramadhani amesema kuwa amejiandaa kumchapa mpinzani wake kutoka Afrika Kusini, Toto Helebe katika pambano la uzito wa Feather.

Wawili hao watavaana kesho Ijumaa (Novemba 04) katika Ukumbi wa Dome Boxing uliopo Masaki jijini Dar es salaam, kwa ushirikiano wa kampuni yenye uzoefu mkubwa wa kuandaa ngumi za kulipwa duniani, Global Boxing Stars kwa ushirikiano na Kampuni ya Tanzania, LP Sport chini ya udhamini wa Azam TV kupitia usiku wa vitasa.

Ramadhan amesema anajua kuwa mpinzani wake amekuja kusaka ushindi, lakini ‘amepotea’ njia kwani amedhamiria kumchapa mapema zaidi.

“Nimejiandaa vilivyo, nawaomba Watanzania waje kwa wingi kunipa sapoti katika pambano hili, ninaahidi sitowaangusha,” amesema Ramadhani.

Mbali ya Ramadhani, bondia mwingine, Shaaban Jongo ametamba kumchapa mpinzani wake kutoka Uganda, Musa Ntege, katika pambano la uzito wa cruiser wa Afrika (ABU) kwa nchi za Afrika Mashariki.

Endapo Jongo atashinda pambano hilo, atapata fursa ya kuwania ubingwa wa Afrika dhidi ya bondia Olanweragu Doradola na kuingizwa katika viwango vya WBC.

Kwa upande wa bondia Salehe Kassim, ameahidi ushindi dhidi ya Mghana Patrick Aryee katika pambano la uzito wa Super Feather.

Wallace Karia: Nitakaa pembeni, Mtanikumbuka

Watanzania wengine, Fadhili Majiha amesema amejiandaa kutoa kipigo kwa mpinzani wake kutoka Ghana, Manyo Plange huku Mohamed Pesa akiahidi kumchapa Tope Tajdeen wa Nigeria katika pambano la uzito wa featherweight. Naye Hamis Palasungulu ametamba kumchapa Solomon Adebayo wa Nigeria katika pambano la uzito wa juu.

Mapambano mengine ya siku hiyo yatakuwa kati ya bondia Paul Kamatha dhidi ya Lemi Madeje wakati Sarafina Julius Bella akizipiga na Sara Alex katika uzito wa fly kwa upande wa wanawake.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa LP Sport, Levis Paul, amesema maandalizi ya mapambano hayo yamekamilika na wanatarajia kuwa na msisimko mkubwa zaidi.

Uzimaji wa moto Kilimanjaro unaendelea: Majaliwa
Ally Kamwe awajibu mashabiki Young Africans