Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewaonya baadhi ya wabunge kutumia usafiri wa bodaboda kwenda katika vikao vya Bunge mjini Dodoma kwamba kitendo hicho ni hatari na kuwaomba kuwa makini.
Amewataka wawakilishi hao wa wananchi kutambua kuwa wanapatikana kwa gharama hivyo lazima wawe makini katika utendaji wao wa kazi.
Ndugai ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Aprili 16, 2021 kutokana na jibu la Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kibaha Vijijini (CCM), Michael Mwakamo.
“Ninazo taarifa baadhi ya wabunge wanakuja bungeni kwa usafiri wa wananchi wa bodaboda (kutoka majumbani mwao kwenda bungeni) na kurudi kwa usafiri wa bodaboda.”
“Ni usafiri mzuri sina shida nao ila nawaomba kuwa makini, kuwa na uhakika na dereva wa bodaboda maana kupatikana kwenu ni kwa gharama kubwa nadhani mmenisoma,” amesema Ndugai akisisitiza kuwa.
Aidha Ndugai ameawaomba wabunge kutafakari kwa umakini kutumia usafiri huo endapo wananchi waliowachagua wakiwaona wakiuutumia inaweza ikaleta picha ambayo siyo nzuri.