Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Prof. Palamagamba John Kabudi, diplomasia ya siasa a kimkakati pamoja na diplomasia ya uchumi vikitajwa kama kipaumbele.

Akizungumza wakati akikabidhi nyaraka na Ilani ya Chama Cha mapinduzi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Prof. Kabudi amesema majukumu na muongozo wa utendaji kazi wa Wizara umetajwa katika ilani ya chama ikiwa ni pamoja na kuifanya sauti ya Tanzania kusikika katika medani za kimataifa, sanjari na kuijenga haiba na taswira ya Tanzania katika jumuiya za kimataifa.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula amemshukuru mtangulizi wake huyo kwa kipindi chote cha miaka miwili alichohudumu katika Wizara hiyo na kuweka misingi imara ya mahusiano na mataifa mengine duniani, ikiwa ni pamoja na kusimamia kikamilifu mikataba yenye tija kwa Taifa na makampuni au mataifa mengine.

Tukio hilo la kukabidhiana Ofisi limefanyika katika ofisi za Wizara zilizopo katika mji wa Magufuli Mtumba Jijini Dodoma na kuhudhuriwa pia na Naibu Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk,Katibu Mkuu, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Mohammed Rajab pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika Tukio jingine aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amekabidhiana ofisi na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Dkt Nchemba ambaye sasa ni Waziri wa Fedha na Mipango na Prof Kabudi ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria kwa pamoja wameahidiana ushirikiano katika kutekeleza majukumu katika Wizara walizopangiwa lengo kubwa likiwa ni kumsaidia Rais Samia kufikia matarajio aliyojiwekea kwa manufaa ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Makamba afunguka kuhusu yanayoendelea baada ya kifo cha Magufuli
Mawaziri wakutana kuweka sawa mambo ya Online TV