Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi – NEEC, limetoa mkopo wa shilingi trilioni 5.6 kwa watanzania milioni 9.8 katika kipindi cha mwaka 2022.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa alipokua akielezea utekelezaji wa majukumu ya Baraza mbele ya waandishi wa habari huku akitoa wito kwa wananchi kuwa na nidhamu ya fedha na kutochukua mikopo endapo hawajajipanga kwa matumizi sahihi ya mikopo hiyo.
Amesema, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi hasa wakina mama wanaochukua mikopo kwa lengo la kufanyabiashara badala yake wanatumia mikopo hiyo kufanya shughuli zingne ambazo sio za kiuchumi na kupelekea mgogoro wakati wa marejesho.
“Elimu inatakiwa kwa wanawake wao wanafikiri kujikwamua kiuchumi ni kwenda kuchukua pesa lakini katika uwezeshwaji tunataka pesa iwe kitu cha mwisho, tumekubaliana na Wizara ya Elimu tutoe elimu ya fedha na tuingize kwenye mitaala kwani tatizo tulilonalo hatusomi kabisa elimu ya fedha,” amefafanua Beng’i.
Aidha, amesema wapo wananchi wanaochukua mikopo na kulipa Ada mashuleni hata kufanyia shughuli za ujenzi wa nyumba bila kujua atarejesha vipi mkopo aliochukua na baadae kusababisha migogoro katika Kurejesha.
Baraza lina majukumu ya kuwezesha kubuni, kupanga, kusimamia, kufuatilia, kutathmini na kuratibu shughuli zote za uwezeshaji wa kiuchumi nchini na linafanya kazi kwa kufuata na kusimamia sera ya Taifa ya Uwezeshaji yenye nguzo mbalimbali ambazo ni Ardhi, Mitaji,Ushirika, Ubinafsishaji Masoko na Ujuzi.