Ushindi wa 3-1 wa Manchester United dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, umemvuta sikio mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Gary Neville ambaye ametoa pendekezo zito.
Gary Neville amedai kuwa kutokana na ushindi huo, haoni namna yoyote ambayo klabu hiyo inaweza kuacha kumpa kazi ya kudumu kocha Ole Gunnar Solskjaer na hata kuchonga sanamu yake kwa heshima.
Solskjaer ambaye alichukua jukumu la kukinoa kikosi cha Man United akipokea kijiti kutoka kwa Jose Mourinho, amefanikisha mengi kwenye Ligi Kuu na hata Ligi ya Mabingwa akiwafuta chozi na kurejesha matumaini kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Jana, timu hiyo ilifanikiwa kufanya maajabu na kuruka vyema kiunzi cha kuingia kwenye mzunguko wa robo fainali wa Ligi hiyo ngumu. Rumelu Lukaku ndiye aliyewalegeza PSG kwa magoli mawili katika dakika ya 2 na dakika ya 30, kabla ya Marcus Rashford kukamilisha safari ya kuingia robo fainali kwa mkwaju wa penati katika dakika za nyongeza, penati iliyoleta mzozo mkubwa.
“Hakuna namna ambayo anaweza asipewe mkataba wa kazi ya kudumu, nadhani ni suala la muda tu,” Neville aliiambia Viasport.
“Hata mechi ya jana ilivyoanza sikuwa na wasiwasi, anaweza akapewa na akaamua hata urefu wa mkataba wenyewe, anaweza kuchagua mshahara wake na anaweza hata akaweka sanamu yake nje ya uwanja… vyovyote atakavyo,” aliongeza.
Manachester United wana kibarua kingine Jumapili ijayo watakapo minyana na Klabu ya Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu. Iko katika nafasi ya nne ikiizidi Arsenal iliyo nafasi ya tano kwa alama moja tu.