Meneja wa klabu ya Newcastle Utd, Steve McClaren amekataa kuwalaumu wachezaji wake baada ya mambo kumuendea kombo usiku wa kuamkia hii leo wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England, kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya wagonga nyundo kutoka jijini London West Ham Utd.

McClaren amesema atakua mchoyo wa fadhila kama ataelekeza lawama kwa wachezaji wake kutokana na kichapo hicho, ambacho kimewashtua wadau wengi wa soka kutokana na muonekano wa kikosi cha Newcastle Utd kwa msimu huu.

Meneja huyo amesema wachezaji wake walicheza vizuri wakati wote na kwa bahati mbaya walijikuta wakipoteza mchezo, hali ambayo kwake haimpi hofu kubwa kwa kuamini bado wana nafasi ya kurekebisha makossa yao katika michezo ijayo ya ligi.

Hata hivyo McClaren amedai kwamba, huenda kikosi chake kilishindwa kutimiza lengo la kupambana na kupata ushindi kutokana na kuchelewa kufika kwenye uwanja wa Upton Park, kufuatia msongamano wa magari uliokua umekithiri jijini London usiku wa jana.

Amesema iliwachukua muda wa dakika 50, kukaa barabarani kabla ya kufika uwanjani hapo, na hawakupata wasaa mzuri wa kupasha misuli joto kikamilifu kabla ya mpambano kuanza.

Katika mchezo huo, mabao ya West Ham Utd yalipachikwa kimiani na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet katika dakika za 9 na 57.

Kwa matokeo hayo Newcastle Utd wamesalia mkiani mwa msimamo wa ligi ya nchini England kwa kuendelea kumiliki point mbili huku West Ham Utd wakifikisha point tisa ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya tano.

Lushoto Kutopiga Kura Ya Ubunge
Djokovic: Nafurahi Kuona Mashabiki Wakiongezeka