Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Zuberi Katwila amesema vijana wake wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wa fainali ya michuano ya CECAFA U20 kesho Jumamosi dhidi ya Kenya, na ana imani kombe litakuja Tanzania.
Tanzania Bara ilifuzu hatua ya fainali baada ya kuifunga Sudan mabao 2-1, wakati Kenya iliishinda Eritrea 1-0 kwenye mechi za nusu fainali. Tanzania Bara na Kenya zilikuwa kwenye Kundi B la mashindano hayo na kwenye mchezo wao wa kwanza walitoka sare ya mabao 2-2.
Tanzania Bara imeyateka mashindano ya mwaka huu kutokana na umakini mkubwa wa safu yake ya ushambuliaji, iliyofunga mabao 17 mpaka sasa, ikiwa ndiyo timu yenye idadi kubwa Zaidi ya magoli ikifuatiwa na Kenya yenye 14.
Katwila ambaye pia ni kocha mkuu wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, amesema maandalizi waliyopata vijana wake ni mazuri na yanawatosha kupambana kwenye mchezo wa fainali, na Mungu akijaalia timu yake kuibuka na ushindi.
“Tunawafahamu Kenya vizuri, tuliwaona hapa wakati wa hatua ya makundi, tunafahamu uzuri na ubovu wao. Kikubwa tumefanyia kazi makosa kadhaa ambayo yalijitokeza kwenye mchezo wa awali ili tuweze kupata ushindi leo.
“Wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri. Bado tuna wasiwasi na Ally Msengi na Frank Kihole ambao ni majeruhi, ila tutaona kama wanaweza kucheza kesho. Tunahitaji kuongeza umakini kwenye safu ya ulinzi pia ili tusiruhusu magoli mengi,” aliongeza kocha huyo bora wa mashindano ya U20 nchini.
Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Dickson Job amesema safu yao ya ulinzi ina kazi nzito ya kufanya hapo kesho ili kuwazuia Kenya, huku akiipongeza safu ya ushambuliaji kwa uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu.
“Tutajitahidi kuongeza umakini kwenye mechi hii, maana ndiyo ya mwisho ya mashindano. Tumekuwa na uwiano mzuri wa kufunga lakini tunatakiwa kuzuia zaidi ili kuweza kupata ushindi,” alisema.
IMEANDALIWA NA GIFT MACHA
AFISA HABARI TANZANIA BARA U20
CECAFA U20 CHALLENGE CUP, UGANDA.