Umoja wa Mataifa (UN), umeonya kuwa njaa na utapiamlo vinaongezeka katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko, ukame na mizozo nchini Sudan Kusini huku baadhi ya jamii zikiwa hatarini iwapo misaada ya kibinadamu haitakuwa endelevu.
Onyo hilo, limetolewa mjini Juba nchini Sudan Kusini na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula duniani, WFP na la kuhudumia watoto UNICEF, yakisema takribani theluthi mbili ya wananchi wa Sudan Kusini, wanaweza kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula kati ya nwezi Aprili na Julai 2023 na watoto milioni 1.4 watakabiliwa na utapiamlo.
Kwa mujibu wa mashirika hayo, kiwango cha utapiamlo kiko katika kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea, kupita viwango vilivyoonekana hata wakati wa vita kati ya mwaka 2013 na 2016 na kwamba kupungua kwa uhakika wa chakula na kuenea kwa kiwango kikubwa kwa utapiamlo kunahusishwa na mchanganyiko wa migogoro.
Taarifa zaidi ya mashirika hayo imeeleza kuwa, pia hali mbaya ya uchumi, majanga ya mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa gharama za chakula na mafuta kunachangia kwa utapiamlo na tayari ufadhili wa programu za kibinadamu umeanza kupungua, licha ya kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu.