Mwanamuziki na mbunge wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana Fa amefunguka kuhusu sakata la baadhi ya wadau wa muziki wakiwamo wasanii nchini Kenya kuanzisha kampeni maalum yenye lengo la kuirudisha hadhi ya muziki wao huku wakiitaka serikali nchini humo kuingilia kati swala hilo ili muziki wa Kenya upewe kipaumbele zaidi kwenye vyombo vya habari kuliko nyimbo kutoka mataifa mengine.

Kufuatia sakata hilo, Mwana Fa ametolea ufafanuzi baadhi ya mambo yanayoendelea kwenye kiwanda cha muziki wa Bongo fleva, akigusia nafasi iliyotengenezwa kiasi cha kuweza kuyashika baadhi ya mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki huku akigusia baadhi ya madhaifu yanayostahili kufanyiwa kazi ili kuufanya muziki wa Bongo fleva kusonga mbele zaidi.

Mwana Fa, ameonesha kutofurahishwa na namna ambavyo baadhi ya Watanzania wamekuwa na utamaduni wa kuwaonyesha heshima na upendo wa hali ya juu wasanii kutoka mataifa mengine hata wakiwa wachanga (Upcoming artists) kwenye mataifa wanatotokea akioanisha hilo na kinachendelea Kenya na hapa nchini.

“Muziki unaweza kupigwa kokote duniani kwa sababu ni lugha ya Dunia, lakini ukweli ni kwamba tulifika mahali tukawa hivi, kama wasanii wa Nigeria hata msanii mdogo ambaye kafanya wimbo wa kawaida akija hapa Tanzania anakuwa Mungu mtu, hiki ndio kitu nilikuwa nakipigania, nakipinga”

“Nashukuru Wakenya wamekuja kukishtukia hiki kitu lakini baadae, miaka kadhaa mbele, na haikuwa vita lakini nafikiri maneno yalifika kwetu hapa kwa hiyo mambo yakarekebishika kidogo, Japo sio kwa jinsi ambavyo mimi ningependelea iwe lakini kwa kiasi fulani hali ilirekebishika “Amesema Mwana Fa

Pamoja na kubainisha hayo Fa, amezichambua tabia halisi za wadau na mashabiki wa Kitanzania, anazodai kuwa ndio chanzo cha kutokuwepo kwa uzalendo wa kutoa vipaumbele kwa wasanii na sanaa ya hapa nyumbani Tanzania.

“Sisi tunatabia ya kurukia rukia sana vitu, hapa kulishakuwa na wakati kuna Kenyan Night in Dar es salam, hiyo hali ni mbaya sana, hao Wakenya tungefika mahali wakawa usiku mzima zinapigwa nyimbo za Kitanzania bila wimbo wa Kenya watakuwa na haki ya kulalamika nafikiri ndio kitu wanachokifanya sasa” Kwamba tufike mahali asilima 75 au 80 ya nyimbo iwe ni local content na hii inatakiwa ifanyiwe kazi kila mahali mpaka kwetu, kila nyimbo kumi zinazopigwa redioni  nane ziwe za Kitanzania.

Maana huu muziki hauwezi kushika kwa bahati mbaya wenyewe, Inatakiwa sababu za kimakusudi, watu wakusudie kwamba tunataka kuusimamisha muziki wetu na hivyo ndivyo inavyojuwa, Nigeria hawakuanza hapo walipo, walihakikisha wanausimamia muziki wao”, ameongeza.

Mwana Fa amewapongeza Wakenya kwa kuanzisha mchakato huo na kutoa rai kwa wadau, wasanii na mashabiki wa muziki nchini, kuhakikisha wanaupigania muziki wao ili kuuweka kwenye nafasi nzuri zaidi itakayo upeleka mbali muziki wa Bongo fleva.

Kamusoko aionya Simba SC
Rais Samia ateta na taasisi za kifedha