Wekundu Msimbazi Simba wanaendelea kujiandaa na mchezo wa mzunguuko wa tisa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara ambao utakutanisha na Wagonga Nyundo wa Jiji La Mbeya (Mbeya City) siku ya jumapili kwenye uwanja wa Kumbukubu Ya Sokoine jijini humo.
Simba wameendelea na mazoezi yao jijini Dar es salaam, huku wakitaka kuendeleza wimbi la kufanya vizuri msimu huu, kwa kukaa kwenye kilele cha msimamo wa ligi, ambapo kwa sasa wamepishana kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Young Africans.
Lakini wakati Simba wakijiandaa na mipango huyo, bado wanakabiliwa na jinamizi la kushindwa kuvuna point sita za michezo miwiwli mfululizo, pindi wanapocheza kwenye uwanja wa Kumbukumbu Ya Sokoine jijini Mbeya, hali ambayo itakwenda kujitokeza tena msimu huu kwa kucheza na Mbeya City kisha Tanzania Prisons.
Changamoto hiyo imeonyesha kumkera kocha mkuu wa timu hiyo ya Msimbazi Joseph Omog, ambapo amesema atahakikisha anatumia mbinu mbadala ili kukabiliana nayo na kufuta rekodi hiyo mbaya dhidi ya kikosi chake.
Kocha Omog ameandaa mpango mkakati maalumu ambao utakiwezesha kikosi chake kuibuka na pointi sita kwenye michezo miwili wanayokwenda kucheza Nyanda za Juu Kusini (Mjini Mbeya).
Akifafanua zaidi Omog alisema amepania kuhakikisha timu yake inavunja rekodi ya Young Africans kwa kushinda mechi hizo mbili ingawa amekiri kuwa siyo jambo dogo.
Akinukuliwa, Omogo ambaye ni raia wa Cameroon alisema: “Msimu uliopita tulijitahidi kufanya hivyo lakini ilishindikana msimu huu tunaanza tena kucheza ugenini mechi zote mbili kwa ubora wa kikosi tulichokuwa nacho naamini tunaweza kuvunja rekodi ya Young Africans.”
Omog amesema anaziheshimu timu za Mbeya City na Tanzania Prisons, lakini msimu huu ataomba wawasamehe kwani wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima na hadhi ya Simba.
Simba wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam siku yoyote kuanzia kesho kuelekea Mbeya, ambapo Jumapili watashuka kwenye Uwanja wa Sokoine kucheza na Mbeya City na baada ya mchezo huo wataendelea kubaki huko mpaka Jumamosi ijayo watakapocheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja huo huo.